Saturday, June 20, 2009

WAZIRI WA ULINZI NCHINI SOMALIA AUWAWA


Waziri wa usalama wa ndani wa Somalia Omar Hashi Aden ameuwawa kwenye shambulio la kujitoa muhanga la bomu lililotegwa kwenye gari kaskazini mwa mji mkuu wa Mogadishu.
Watu wengine zaidi ya 20 wameuwawa kwenye mlipuko huo katika Hoteli ya Beledweyne, kaskazini mwa mji mkuu wa Mogadishu.

Miongoni mwa waliouwawa ni maafisa kadhaa wa Kidiplomasia wa Somalia.

Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed amelaumu kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Al-Shabaab , ambalo pia baadaye lilikiri kufanya shambulio hilo.

Kundi hilo linaaminika kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al -Qaeda.

Siku ya jumaatano watu 10 walikufa wakati kombora liliporushwa kwenye msikiti mjini Mogadishu.

Katika shambulizi la Alhamisi , walioshuhudia walisema mlipuaji wa kujitoa muhanga alilipua gari lililojaa mabomu kwenye hoteli ya Medina , mjini Beledweyne, yapata Kilomita 400 kaskazini mwa Mogadishu.

Abdulkarim Ibrahim Lakanyo, balozi wa zamani wa Somalia nchini Ethiopia pia ameripotiwa kuwa miongoni mwa waliouwawa.

Mwandishi wa BBC Will Ross anasema bwana Aden alihamia mjini Beledweyne hivi majuzi, mji ulioko karibu na mpaka wa Ethiopia, katika jitihada za kukomesha wanamgambo wa Kiislamu wasiendelee kuthibiti maeneo mengi zaidi.

Rais Ahmed ameambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Mogadishu kwamba Somalia imevamiwa na magaidi wasiotaka kuona benderea ya nchi hiyo, wala amani .

Amesema kundi hilo la Al- shabaab linajificha kwenye Uislamu kuendesha ukatili wao.

Somalia haijawa na serikali dhabiti tangu mwaka wa 1991 , na zaidi ya watu milioni nne , ambao ni asilimia 75 ya raia wa nchi hiyo wanahitaji msaada wa chakula.

Kundi la Al- Shabaab ni mshirika katika muungano wa wanamgambo wa kiislamu wenye msimamo mkali ambao wamekuwa wakijaribu kuiangusha serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na umoja wa mataifa.

Rais Ahmed , ambaye mwenyewe ni muislamu mwenye msimamo wa wastani alichukua khatamu nchini Somalia mwezi Januari , lakini hata baada ya kuanzisha utawala wa kuzingatia sheria za kiislamu , hatua hiyo bado haijawaridhisha wapiganaji hao.

Jumaatano , kamanda mkuu wa Polisi mjini Mogadishu aliuwawa kwenye mashambulizi dhidi ya ngome za wanamgambo.

Mwakilishi wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi UNHCR nchini Somalia amesema umwagikaji damu wa hivi karibuni nchini Somalia ndio mbaya zaidi kuikumba nchi hiyo kwa muda wa karibu miaka 20.

No comments: