Saturday, June 20, 2009

WAANDISHI WA HABARI MARUFUKU KUTANGAZA BEI ZA VIUNGO VYA ALBINO VINACHOCHEA MAUAJI YAO NCHINI TANZANIA


Na Sharon Sauwa
Washiriki wa mkutano wa kujadili mauaji ya albino, wamevitaka vyombo vya habari kutotangaza bei ya viungo vya walemavu hao.
Wamesema kufanya hivyo kunachangia kuhamasisha mauaji ya albino kwa kuwashawishi watu kufanya biashara ya namna hiyo.

Walitoa ushauri huo walipokuwa wakiwasilisha majadiliano ya vikundi jijini Dar es Salaam jana.

Hali kadhalika, wameitaka serikali kuweka wakaguzi katika maduka ya kuuza dawa za asili kama wafanyavyo katika maduka ya dawa za viwandani.

Walisema kuwa kufanya hivyo kutawawezesha kubaini iwapo dawa wanazouza haziendi kinyume na kanuni na sheria za nchi.

"Kwenye maduka haya asiyekuwa na ujuzi wa dawa za kienyeji, anauza tu ama dereva teksi anaweza naye leo hii akafungua duka la dawa za asili na anakubalika," alisema mmoja wa washiriki wa semina hiyo, Rose Abdallah.

Walisema hakuna watu wanaofahamu kinachouzwa katika maduka hayo hali inayowafanya baadhi yao kuuza viungo vya wanyama wakidai kuwa vinatumika katika kuponya magonjwa mbalimbali.

No comments: